Exodus 12:3-21

3 aIambie jumuiya yote ya Israeli kwamba katika siku ya kumi ya mwezi huu, kila mtu atatwaa mwana-kondoo mmoja kwa ajili ya familia yake, mmoja kwa kila nyumba. 4Ikiwa nyumba yoyote ina watu wachache wasioweza kumaliza huyo mwana-kondoo mzima, nyumba hiyo itabidi ishirikiane na nyumba ya jirani wa karibu, baada ya kuzingatia idadi ya watu waliomo. Mtaangalia ni kiasi gani cha nyama kitahitajika kulingana na mahitaji ya kila mtu. 5 bWanyama mtakaowachagua, lazima wawe wa kiume wa umri wa mwaka mmoja wasiokuwa na dosari, mwaweza kuwachukua kati ya kondoo au mbuzi. 6 cTunzeni wanyama hao mpaka siku ya kumi na nne ya mwezi, ambapo lazima watu wa jumuiya yote ya Israeli wachinje wanyama hao wakati wa jioni. 7 dNdipo watakapochukua baadhi ya hiyo damu na kuipaka kwenye vizingiti vya juu na miimo ya milango ya nyumba ambamo watakula wana-kondoo hao. 8 eUsiku huo huo watakula nyama iliyookwa kwenye moto, pamoja na mboga chungu za majani na mikate isiyotiwa chachu. 9 fMsile nyama mbichi wala iliyochemshwa, lakini iwe imeokwa kwenye moto, kichwa, miguu na nyama zake za ndani. 10 gMsibakize nyama yoyote mpaka asubuhi; nazo kama zitabakia mpaka asubuhi, lazima mziteketeze kwa moto. 11 hHivi ndivyo mtakavyokula: Mtajifunga mikanda viunoni, mtakuwa mmevaa viatu vyenu miguuni na kushika fimbo zenu mkononi mwenu. Mle kwa haraka; hii ni Pasaka ya Bwana.

12 i“Usiku huo huo nitapita katika nchi yote ya Misri na kumuua kila mzaliwa wa kwanza, wa wanadamu na wa wanyama, nami nitaihukumu miungu yote ya Misri. Mimi ndimi Bwana. 13 jDamu itakuwa ishara kwa ajili yenu ya kuonyesha nyumba ambazo mtakuwamo; nami nitakapoiona damu, nitapita juu yenu. Hakuna pigo la uharibifu litakalowagusa ninyi nitakapoipiga Misri.

14 k“Siku hii itakuwa kumbukumbu kwenu, mtaiadhimisha kuwa sikukuu kwa Bwana, katika vizazi vyenu vyote: mtaishika kuwa amri ya kudumu. 15 lKwa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu. Katika siku ya kwanza mtaondoa chachu yote ndani ya nyumba zenu, kwa maana yeyote atakayekula chochote chenye chachu kuanzia siku ya kwanza hadi ya saba lazima akatiliwe mbali kutoka Israeli. 16 mKatika siku ya kwanza mtakuwa na kusanyiko takatifu, na kusanyiko jingine katika siku ya saba. Katika siku hizo msifanye kazi kamwe isipokuwa kutayarisha chakula cha kila mmoja; hilo ndilo tu mtakalofanya.

17 n“Mtaadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, kwa sababu hiyo ndiyo siku ile niliyovitoa vikosi vyenu kutoka Misri. Mtaiadhimisha siku hii kwa vizazi vyenu vyote kuwa amri ya kudumu. 18 oKatika mwezi wa kwanza mtakula mikate isiyotiwa chachu, kuanzia jioni ya siku ya kumi na nne hadi jioni ya siku ya ishirini na moja. 19 pKwa muda wa siku saba isionekane chachu yoyote katika nyumba zenu. Yeyote alaye chochote chenye chachu ndani yake, lazima akatiliwe mbali kutoka jumuiya ya Israeli, akiwa ni mgeni au mzawa. 20 qMsile chochote kilichotiwa chachu. Popote muishipo, ni lazima mle mikate isiyotiwa chachu.”

21 rNdipo Mose akawaita wazee wote wa Israeli na kuwaambia, “Nendeni mara moja mkachague wanyama kwa ajili ya jamaa zenu, mkachinje mwana-kondoo wa Pasaka.
Copyright information for SwhNEN